Monday, April 27, 2009

Wanafunzi washupalia mauaji ya maalbino 2009-02-15 12:47:50 Na Mwandishi Wetu
Wanafunzi wanachama wa chama cha kutetea haki za binadamu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, wamesema watatumia nafasi yao katika jamii kufanya mabadiliko ya kumaliza ukatili nchini kwa kuishinikiza serikali kuongeza kasi ya kudhibiti mauaji ya maalbino. Rais wa chama hicho, Onesmo Ngurumwa, aliyasema hayo jijini Dar es Salaam jana wakati wa mdahalo maalum uliojadili mauaji ya maalbino ulioandaliwa na chama hicho kwa kushirikiana na chuo kikuu kishiriki cha kimataifa cha mafunzo ya sheria cha Ujerumani. Alisema pamoja na kwamba mauaji ya maalbino yameendelea kutokea kila mara, serikali imeshindwa kushughulikia tatizo hilo kwa kasi inayostahili. Alisema ili kufanikisha mabadiliko wanayokusudia, wapo katika mkakati wa kuandaa mapendekezo ya namna ya kukabiliana na mauaji hayo ambayo watayapeleka serikalini ili yafanyiwe kazi. ``Tutabuni mikakati itakayosaidia kutokomeza ukatili wa binadamu hasa mauaji ya albino na tutayawasilisha kwa wadau ikiwemo serikali ili yafanyiwe kazi,`` alisema Ngurumwa. Mkurugenzi wa uhariri wa magazeti ya IPP, Sakina Datoo, alisema vyombo vya habari vina nafasi kubwa ya kupambana na ukatili huo. Amewataka waandishi kuendelea kuandika habari za uchunguzi kuhusu mauji ya maalbino na kuwafichua wauaji ili kutokomeza vitendo hivyo. ``Kama mnakumbuka, vyombo vya habari ndivyo vilivyofichua mauaji haya, kwa hivyo ninaamini bado waandishi wa habari wanao mchango mkubwa sana katika hili,`` alisema.
SOURCE: Nipashe
Habari za Leo

No comments: