Tuesday, October 11, 2011

Msekwa Atolewe Ngorongoro

Wasomi wa Ngorongoro Walivalia Njuga Suala la Msekwa na Telele
Hivi karibuni Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mzee Pius Msekwa alitoa utetezi wake katika gezeti la Mwanahalisi kuhusiana na sakata la Hifadhi ya Ngorongoro, sisi wasomi wa Ngorongoro tuona utetezi huo ni dhaifu na tunaomba kumfahamisha Mzee wetu huyo msimamo wetu.
Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ni mamlaka iliyoanzishwa kwa sheria ya Hifadhi ya Mamlaka ya Ngorongoro ya 1959 (Sura 284 ya sheria za Tanzania) tarehe 1, Julai 1959.Sheria hii ni wazi ni sheria ya wakoloni.Tukumbuke kuwa sheria zote zilizotungwa kipindi cha mkoloni zilikuwa zimelenga kutoa mwanya mzuri wa wakoloni kutawala bila kupata pingamizi lolote toka kwa wazawa.
Sheria hii inasema wazi wazi kuwa mamlaka ya Ngorongoro ipo kwa ajili kulinda rasilimali pamoja na jamii ya kimasai inayoshi katika eneo la hifadhi.Sheria hii katika kifungu cha 5 na kama ilivyoelezewa wazi katika vifungu vya ziada (Second schedule) inatamka kuwa Bodi ya mamlaka ya Ngorongoro ndio itakuwa chombo kikubwa cha maamuzi katika uendeshaji wa mamlaka ile.

Pia inatamka kuwa wajumbe wa bodi watateuliwa na waziri wa wizara husika isipokuwa Mwenyekiti wa bodi ambaye anateuliwa na rais.Sheria hii ya kikoloni ina mapungufu makubwa na ndiyo chanzo cha mgogoro wa Mh Kaikai Telele na aliyekuwa waziri wa wizara ya mali asili Shamsa Mwangunga na aliye mwenyekiti wa sasa Pius Msekwa.

Waliopata kuwa Wabunge Ngorongoro miaka ya nyuma kuanzia mpiganaji Moringe Ole Parkipuny, Richard Ole koilah na Methew Ole Timan walikuwa wajumbe wa bodi, iweje leo Mh.Telele awekwe Pembeni?Hapa kuna agenda ya siri na hujuma kwa wanangorongoro, kwa maana hiyo mh. Telele yuko sahihi kusema Msekwa anahujumu Ngorongoro.
Mbunge wa wilaya ya Ngorongoro sio mjinga na wala sio msongombingo bali ni mzalendo na alieyamua kuweka wazi madudu yanayofanyika katika mamlaka ile ya Ngorongoro. Basi kama kuna mtu atamuita Telele mzushi na mjinga atakuwa amewatukana Wanangorongoro wote kwani yule ni mwakilishi wa wananchi na ana haki ya kusema chochote anachokiona kinapelekea kupotea kwa haki za Wanangorongoro.
Shamsa Mwangunga alitumia ubovu wa sheria hii ya kikoloni kumtoa Mbunge wa Ngorongoro kwenye ujumbe wa bodi ya Ngorongoro. Upo ushahidi usiopingika kwamba Mh.Telele alitolewa kwenye ujumbe wa Bodi ya Mamlaka kwa chuki binafsi.Tukumbuke kwamba Bodi hiyo ya mamlaka ndiyo hupitisha na kupanga miradi mbalimbali ndani na nje ya hifadhi.
Miradi hiyo pia huhitaji ushirikishwaji wa wenyeji.Sasa je kama mwakilishi wa wilaya amefukuzwa ujumbe na nafasi yake kupewa mbunge mwingine aneyetoka jimbo jingine ni nani atakuwa msemaji halali wa wananchi katika maamuzi mbalimbali? Je Telele akisema walimtoa makusudi ili wawe huru kufanya ufisadi wao kama ilivyoonekana katika uwekezaji wa hoteli na shughuli zingine za mamlaka atakuwa ni mzushi? La hasha atakuwa mzalendo na jasiri katika kukemea maovu.
Mbunge anapaswa kuwa mjumbe ili kuzungumzia maslahi na matatizo ya Wanangorongoro. Mfano, swala la ajira kwa jamii ya kimasai wanaoishi ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro imekuwa finyu sana, kati ya wafanyakazi 448, wamasai au wenyeji ni 75, kati ya hawa asilimia 98 ni walinzi wa wanyamapori, wafanyakazi wengi wanaoajiriwa na mamlaka ya hifadhi hiyo ni ndugu wa karibu wa wakurugenzi wa idara mbalimbali za mamlaka, wajumbe wa bodi na wengine wanaotoka Kanda ya Ziwa toka enzi za Mhifadhi Cheusi wakiingia ofisini kwa memo kutoka kwa wakubwa.

Wananchi wanaoishi ndani ya hifadhi ya ngorongoro wamekuwa fukara kupindukia , watoto wanashindwa kwenda shule kwa sababu ya njaa, wengi wao wanaenda kuokota mabaki ya unga kwenye mashine ili waweze kujikimu, upande mwingine mamlaka ya hifadhi ya ngorongoro wakitumia fedha nyingi kwa ajili ya safari za nje, kwa mwaka wa fedha 2011/2012 mamlaka ilitenga sh 3.1bilion kwa ajili ya kwenda kutangaza utalii kama wanavyosema lakini kwa takwimu tulizonazo kutangaza utalii kwao haijawahi ongeza idadi ya watalii wanaoingia kwenye hifadhi.

Kinachoshangaza ni wakurugenzi wa idara ndio wanaenda nje kutangaza utalii badala ya maafisa utalii ambao ndio nyenzo kubwa kama wangetumika. Tokea Mzee Msekwa alipoteuliwa kuwa mwenyekiti wa bodi ya mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro amekuwa msumari wa moto kwa wenyeji, kuanzia ajira, elimu na maendeleo mengine ya kijamii.kabla ya kuteuliwa kwake kuwa mwenyekiti wa bodi ya mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro wenyeji walipata fursa ya kupatiwa elimu kutoka shule za sekondari mpaka vyuo vikuu bila vikwazo kupitia baraza la wafugaji,

Lakini baada ya Mzee Msekwa kuwa mwenyekiti wa bodi alitoa agizo kwamba watoto wa kimasai wasisomeshwe tena vyuo vikuu kwa sababu kuna bodi ya mikopo, lakini Watanzania wenzangu wanaweza kukubaliana na mimi kuwa bodi ya mikopo haitoshelezi kuwasomesha wanafunzi wote wanaojiunga na vyuo vikuu Tanzania na pia ikumbukwe lengo kubwa la Mamlaka ile ilikuwa ni kuwasaidia wamasai wanaoshi katika bonde lile samba samba utunzaji wa uridhi huo wa dunia.

Aidha Mzee Msekwa huyo huyo aliona kuwa hilo halitoshi akaongeza kikwazo kingine kuwa wanafunzi wanaosomeshwa na baraza la wafugaji shule za sekondari wasilipiwe tena kwenye shule binafsi kwa kigezo kuwa wanalipiwa fedha nyingi na kutoa agizo kuwa wasomeshwe shule za kata tu ambazo kwa sasa tunaita vyuo vya kukuzia watoto na sio shule kwani wengi wao hutoka na alama sifuri. Kwa sasa watoto wengi wa kifugaji hawaendi shule tena na waliopo vyuo vikuu nao kwa mwaka huu wa masomo hawana fedha za kujiunga na vyuo.

Mh. Kaika Oletelele alipokuwa kwenye bodi hiyo alijaribu sana kutetea kwa hali na mali maslahi ya wenyeji na kwa kiasi kikubwa alifanikiwa kuwabana akina Mzee Msekwa kwa hoja.Lakini wakubwa hao ili kutimiza maslahi yao walimshawishi Waziri Mwangunga kwa wakati huo kumtoa Mh telele kwenye bodi hiyo kwa kigezo tu kwamba alikuwa akitetea maslahi ya wenyeji.
Kwa ujumla mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro kuanzia Bodi hadi utawala imeashiria kuchafuka kwa tope la rushwa na ubaguzi. Mamlaka hiyo imegeuka kuwa taasisi ya watu fulani wakilindwa na viongozi wa juu.Kila mwishoni mwa mwaka viongozi wa juu wa nchi huja kupumzika katika hotel za kitalii na familia zao kwa gharama za hifadhi. Mamlaka sasa inaendeshwa kichama, kwanini kiongozi wa chama ndio Mwenyekiti wa Bodi halafu Mwakilishi wa wananchi anatupwa pembeni? Kazi ya Bodi ni kupitisha miradi lakini Msekwa sasa kageuka msimamizi wa miradi mbalimbali ili kuendelea kuvuna posho toka mamlaka ya Ngorongoro.

Makamu huyu wa mwenyekiti wa CCM kaendeleza sera za kuwaondoa wafugaji na kuwakataza kilimo cha kujikimu. Kihistoria kilimo cha kujikimu ndani ya bonde la Ngorongoro iliruhusiwa mwaka 1991 na aliyekuwa waziri mkuu kwa wakati Mzee John Malecela kwa kuwaonea huruma wenyeji hao waliokuwa wamekumbwa na njaa kubwa sana. Kwa sasa wananchi hawa wana hali ngumu kimaisha kutokana na utekelezaji wa sera hizi kandamizi.

ukilinganisha maisha ya wenyeji wa Ngorongoro wakati walipokuwa na kilimo cha kujikimu na kwa sasa miaka miwili tu baada ya kukatazwa imekuwa mbaya sana, wenyeji walikuwa wakitumia mifugo kuwapeleka watoto shule lakini kwa sasa imekuwa tofauti, mifugo inauzwa kwa ajili ya chakula badala ya kutumiwa kuwapeleka wanafunzi shule, matokeo yake wengi wanakaa nyumbani ukizingatia pia na Baraza kwa sasa halipewi tena pesa za kutosha kwa ajili ya elimu.

Hatima ya wananchi wale ni mbaya sana, inasikitisha, wengi wao wamekumbwa na magonjwa ya utapiamlo, watoto wanaolazwa kwenye hospitali ya Endulen asilimia 95 wanaugua magonjwa yanayotokana na utapiamlo.Wakati tunasherehekea miaka 50 ya Uhuru wananchi wa Ngorongoro wanasherehekea miaka 53 ya mateso na umaskini, hasa waliopo ndani ya bonde hilo bila kuwa na dalili za kufurukuta.

Mbunge wa Ngorongoro anapaswa kuwa mjumbe wa Bodi ya Mamlaka ya Ngorongoro kwa mujibu wa nafasi yake ya uwakilishi.Sheria hii imempa nguvu za ziada waziri kufanya anachotaka.Tunawasihi wabunge wengine wote waungane na sisi wasomi wa Ngorongoro kupigania sheria mpya ya mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro.
Sheria inapaswa kutamka wazi wazi kuwa Mbunge wa Ngorongoro atakuwa mjumbe kwa kupitia kofia ya ubunge.Vile vile tunamwomba Rais Kikwete amrudishe Mh.Telele kwenye Bodi ya Ngorongoro na Kumtoa Mzee Msekwa. Tunamsihi kigogo huyo wa chama tawala ajue kuwa Telele hamuonei wivu kwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi bali kiuhalisia na kisheria Mh Telele kama mbunge wa Ngorongoro anapaswa na ana haki kuwa mjumbe wa bodi kwa ajili ya kuwawakilisha wanangorongoro.

Waadishi wa Makala hii ni Wanaharakati na Viongozi wa Mtandao wa Wasomi Ngorongoro(NDUSA) Onesmo Olengurumwa opngurumwa@gmail.com na Emanuel Oleshangai -0713996908