Wednesday, June 29, 2011

Serengeti High Way -“Kanuni ya Uhuru wa Nchi Kutumia Maliasili Hatarini"

SEHEMU YA TANO
Mpendwa Msomaji, baada ya kusoma toleo la nne na kuweza kuona misimamo ya viongozi wa Kitaifa kuhusiana na sakata hili la barabara.Makala hii inakuletea msimamo wa Wizara ya Maliasili kuhusiana na ujenzi wa barabara ya kuu ya kutoka Arusha hado Musoma kupitia Loliondo.Hivi karibuni Waziri wa Maliasili Ezekiel Maige alimwandikia barua ya msimamo wa Wizara, Mkurugenzi wa Shirika la Utamaduni na Maliasili Duniani(UNESCO).Barua hiyo ya tarehe 22/5/2011 ni kama vile ilikuwa inajibu matakwa ya UNESCO. Kichwa cha Habari hiyo inajibu malalamiko na vitisho vya UNESCO na mataifa tajiri dhidi ya mpango wa serikali ya kujenga barabara kwa watu wake.

Barua hiyo inaelezea jinsi serikali ilivyoshindwa kusimamia msimamo wake wa kujenga barabara kuu ya kuwaunganisha watu wa kanda ya ziwa na mikoa ya Kasakazini kiuchumi. Hapo awali malengo ya Serikali yalikuwa ni kuwaunganisha wanachi wa mikoa hiyo kiuchumi. Lakini kwa mujibu wa barua ya Waziri Ezekiel Maige kwa UNESCO mpango huo umekufa kifo cha taratibu wanachi wamepumbazwa kuhusiana na hili.Ukweli ni kwamba mpango wa serikali wa kujenga barabara toka Musoma hadi Arusha kupitia Loliondo haupo tena na badala yake kitakachotekelezwa na mipangao ya UNESCO, Frank Foot Zoological Society, WB na Nchi kama Ujerumani na Kenya.Njia ya kaskazini(Nothern route) ndugu watanzania haupo tena na kinachofanyika sasa ni kujenga barabara za wilaya 3 Serengeti, Monduli na Ngorongoro.Najaribu kuitafsiri barua hiyo kama ifuatavyo; Mpango wa barabara kwa sasa umegawanyika mara mbili, ukanda wa mashariki ambao upo ndani ya Ngorongoro barabara itajengwa kwa kiwango cha lami toka Mtoambu hadi Loliondo kupitia Ziwa Natron kwa urefu wa kilometa 214 , upande wa mashariki ambao upo wilayani Serengeti watajenga kilometa 117 toka Makutano-Natta-Mugumu na sehemu ya katikati toka Mugumu hadi Loliondo kama umbali wa kilometa 100 haitajengwa kwa kiwango cha lami.

Kwa uchambuzi wa harakaraka ni kwamba serikali imezidiwa kete na mataifa makubwa.Je ule mpango wa kuwaunganisha watanzania wa kanda ya ziwa na wa kaskazini bado upo? La hasha haupo tena, mkubwa akipigwa halii, serikali haitaki kusema ukweli.Iweje leo waseme zile kilometa 53 zitabaki chini ya Usimamizi wa TANAPA.Je Loliondo hadi Lolosokwani ipo chini ya Tanapa.Je barabara hizi tutaziita tena High way-Njia kuu? la hasha ni barabara za ndani za wilaya na huu ndio mpango uliokuwa wa Nchi kama ya Ujerumani.

Ule mpango wa kiuchumi sasa umekufa, barabara kwa sasa itawasaidia tu wanachi wa wilaya zile kwenda Arusha Mjini kirahi lakini sio kufungua fursa nyingi za kiuchumi.Mpango huu unaweza kuwa umeleta ushindi sawa ( Win win situation) kama wengine wanavyosema.Wanaojiita Watetezi wa maliasili watakuwa wameshinda zaidi na ndio maana wengine wamejitangaza wameshinda vita vya serengeti.Nasema hakuna fursa sawa kutokana na kwamba bado wale wananchi wa wilaya zile wataendelea kubaki wenyewe bila muunganiko wowote.Na pia haiwezi kuwa win win situation(fursa sawa) kwa sababu yale malengo ya serikali ya kujenga barabara kuu (High way) yametoweka.

Kwangu mimi binafsi naona ni udhaifu mkubwa kwa serikali ya nchi huru kama Tanzania.Hapa kuna tatizo la kuongozwa na mataifa makubwa katika mambo ya msingi ya Taifa letu.Hii hatuwezi sema kuwa ni win win sutuation ilhali uhuru wa Taifa letu unachezewa.Maamuzi ya Taifa letu yanapaswa kutekelezwa bila kuingiliwa na Taifa au Shirika lolote.Tabia hii ikizoeleka hakika tutukuwa taifa mfu ambalo kila tunalolipanga tunahitaji kupewa ruksa au laa na mataifa makubwa na wakati mwingine mashirika ya kimataifa.Ugonjwa huu tunatakiwa tuukemee kwa nguvu zote.
Mwishoni wa Aprili mwaka huu Mkurugenzi wa Benki ya Dunia wa nchi za Africa Mashariki, pamoja na viongozi wengine wa serikali walikuwa eneo la Loliondo hasa kata ya Soit na kuwaahidi wanachi wale kuwa barabara itajengwa.Sasa inakuwaje leo barua ya waziri wa maliasili ikinzane na watu wa TANROAD. Je barua ya Waziri Maige ni Msimamo wa Serikali au wizara? Tukumbuke kuwa ujenzi wa barabara upo nchini ya Wizara ya Ujenzi kitengo cha wakala wa barabara (TANROAD). Hata hivyo taarifa zingine zinaonyesha kuna watu katika wizara hizi mbili hawaungi mkono hoja ya serikali kuwa na barabara kuu inayowaunganisha wanachi wa kanda ya Ziwa na wananchi wa mikoa ya kaskazini kiuchumi.Hii ni changamoto kwa ustawi wa nchi kama hizi ambazo ni changa kiuchumi.Watu wote wanapaswa kuwa wazalendo pale serikali inapokuwa na mipango ya kuinua watu kiuchumi.Mipango ya maendeleo haipaswi kupingwa kabisa bali kusahishwa.Mfano mipango kama MKUKUTA wengi hatuupingi bali tunakosoa na kutoa mawazo nini kifanyike mafanikio ya kweli yaonekane.

Hivi karibu mikutano mingi ya UNESCO imefanyika na suala ya barabara ya Musoma –Arusha ilikuwa gumzo.Pia baadhi ya viongozi wetu toka wizara ya Ujenzi wamekwenda Ujerumani kueleza msimamo wa serikali kuhusu barabara hiyo.Je wamekwenda kutoa ufafanuzi au kusihi Ujeruman wakubali mpango wa barabara.Tatizo la umaskini limekuwa chanzo kikubwa cha nchi za ulimwengu wa tatu kutokuwa na uhuru wa kijiamualia mambo yake ya msingi.Kutokana na ukweli kwamba fedha zitatoka kwa hao hao wanaopinga mpango wa serikali. Tusubiri kwa hamu nini kilichojiri huko Ujerumani.

Nadhani inafika mahala nchi hizi zifikirie namna ya kujikwamua kiuchumi ili kuondokana na utegemezi unaotudhalilisha. Nchi hizi omba omba kama Tanzania hakika hatuwezi kufanya lolote kinyume na matakwa ya wahisani.Ni ukweli usiopingika kuwa hatuko huru kiuchumi na hasa upande wa mali asili.Na ili tuepukane na hili pia nchi inaweza kutumia nchi zingine kama China, Japan, Russia na Korea kuondesha miradi mingine ya kimaendeleo na sio tu nchi za magharibi. Mimi naamini zipo nchi nyingine zingeweza kujenga barabara hapa nchini bilaa kuleta masharti magumu.


Hivyo ndoto ile ya kufanya mikoa ya kanda ya ziwa kuwa pamoja kiuchumi na mikoa ya kaskazini na kwa kupitia barabara kuu ya Musoma- Arusha kupitia Loliondo sasa haipo tena.Kuwepo kwa barabara ile ingeuwa soko la Nairobi na wilaya za Kenya jirani na Tanzania ambapo kwa sasa ndio hutumika zaidi na wanachi wa mipakani.Pengine ndio maana Kenya ndio nchi pekee ya Africa Mashariki iliyoonekana kupinga mpango wa barabara hii.

Na Onesmo Olengurumwa-Mtafiti na Mwansheria LHRC, Pia ni Makamu wa Rais Mtandao wasomi Ngorongoro.Opngurumwa@gmail.com

Sunday, June 5, 2011

Serengeti High Way Part 4




________________________________________
Sehemu ya Nne
Wapendwa wasomaji, kama nilivyowahadi toleo la leo limelenga kukupa habari za hivi karibuni toka wilaya zinazopakana na Hifadhi ya Serengeti.Mapema Mei mwaka huu Bodi ya barabara ya Mikoa ya Arusha na Mara walikutana na wadau wa Mamlaka ya Hifadhi Tanzania(TANAPA) na kukubaliana kuwa ni lazima barabara hiyo ijengwe kama vile serikali ilivyopanga lakini kwa kuzingatia ulinzi wa mazingira.Wakizungumza wakati wa mkutano wa Bodi hiyo ya barabara Meneja wa TANROAD , Bwana Desdatus Kaboko alisisitiza kuwa kuanzia January tayari wameshaanza kukusanya pesa za mradi huu na wanategemea uanze rasmi mwaka 2012.Mkutano huo ulionyesha kuwa barabara ile ni muhimu sana kwa mapinduzi ya kiuchumi kwa wakazi wa mikoa hiyo na kanda ya ziwa.Pia TANAPA ambayo awali ilikuwa inapinga mpango wakati huu inaonekana kuwa pamoja na serikali katika juhudi za kuwakwamua wananchi kimaendeleo bila kuharibu mali asili yoyote.
Tarehe 31 mwezi Mei 2011 Mkurugenzi wa Benki ya Dunia Tanzania na Uganda Bwana John Murray pamoja na Mwakilishi wa Balozi wa Ujerumani ,Gisela Habel walitembelea wilaya ya Ngorongoro na Kufanya mikutano na wananchi wa Wilaya ya Ngorongoro.Mwakilishi huyu aliongozana pia wataalamu wa barabara na mazingira wa bank hiyo, viongozi toka wizara ya Ujenzi na viongozi wa TANROAD Mkoa wa Arusha.
Bahati nzuri nami nilikuwepo Wilayani Ngorongoro kwa shughuli mbalimbali na kuweza pata taarifa hizi kwa undani.Wananchi wa Wilaya hii japo sio wote walifanikiwa kufanya mkutano na viongozi hao na kueleza dukuduku zao.Lengo la ziara hiyo ilikuwa ni kupata mawazo ya wananchi juu ya barabara ya Musoma -Loliondo hadi Arusha.Mkutano huo ulifanyanyika katika Kijiji cha Soit sambu-loliondo.Msafara huo ulipokelewa na mabango yanayosisita kuwa barabara ya lami ni muhimu kwa maendeleo ya wanangorongoro.Baadhi ya Mabango ya hayo yakuwa na ujumbe ufuatayo;

"Huduma hi ya barabara itasadia huduma mbalimbali za maendeleo kama vile zahanati, shule na Afya"

Pia bango lingine lilijidadi kuwa; " Tunahitaji barabara ya lami wa maendeleo ya wanangorongoro"
Wananchi wengi walimweleza Mkurugenzi huyo kuwa barabara ya lami ni muhimu kwa maendeleo hasa hupatikanaji wa masoko ya mifugo na biashara zingine.Wanachi hao walionyeshwa kukerwa na watu wanaopinga barabara ambao ni mpango wa serikali kuwakwamua wananchi wake kiuchumi.Waliwalaani wale wote hasa wanaotoka mataifa ya nchi na kupinga mpango huu wa barabara.




Wanagorongoro wakimpokea Mkurugenzi wa World Bank kwa Mabango

Nao viongozi mbalimbali wa wilaya hasa madiwani walieleza kuwa hatuko tayari kuona maslahi ya wananchi yakibinywa na wachache wenye maslahi binafsi.Diwani wa Soit Sambu Daniel Ngoitiko alionekana kukerwa na wanaharakati pamoja na mashirika ya nje yanayopinga barabara ilihali katika nchi zao barabara za lami zimepita katika mbuga zao.Mhe Daniel Ngoitiko aliendelea kuitaka serikali isiyumbishwe na kelele za mashirika pamoja na nchi mbalimbali zinazotaka kupindisha barabara hii ipite mahali kwingine.Kwa ujumla wananchi na viongozi wao wilayani Ngorongoro wamesema barabara ni haki yao na hakuna mtu yoyote anaeweza pinga mpango huo ambao uberakiwa na Bunge la Tanzania na madiwani wa Mikoa yote inayozunguka hifadhi ya Serengeti.

Walindelea kusema kwa sasa hatutakubali kuona wananchi wa wilaya hizi tunaendelea kuachwa nyuma kimaendeleo wakati wengine wanazidi kusonga mbele kimaendeleo.Walinukuu katikaba na kusema katiba ya Tanzania inasema Taifa linajukumu ya kutoa fursa sawa za maendeleo kwa watu wake
bila ubaguzi au upendeleo na rasilimali za nchi zitumike sawa kuleta maendeleo kwa wote.Wananchi hawa waliendelea kusema "tumenyasasika na kusahaulika kwa muda mrefu lakini leo baadhi ya watu wachache wanataka hata barabara tusipate" alisema mmoja wa wanavijiji

Ukweli ni kwamba wanachi wale wanahitaji vichocheo vya maendeleo kama vile barabara na umeme ili kuwatoa kwenye lindi la umaskini.Wanachi wale wametunza maliasili yote, lakini leo hawathamniki tena wanaitwa wakenya na wavamizi.Sasa inakuwaje leo msimame na kupinga barabara ambayo inaweza kuwa chanzo cha mabadiliko.Hakika mnaopinga barabara ya Musoma-Arusha hamna nia njema na wananchi wa wilaya hizi zilizoachwa nyuma kimaendeleo.

Naye mwakilishi wa WB Tanzania aliwaeleza wananchi wale kuwa hana tatizo na barabara hii na Benki ya Dunua ipo tayari kusaidia kama ni vipaumbele vya wanachi na Taifa lake.Pia viongzi wengine wa kitaifa akiwemo Meneaja wa TANROAD Arusha aliwaakishia kuwa mpango wa barabara bado upo pale na hakuna atayeweza kuutengua.
Ni wazi kuwa jamii hizi kwa miaka mingi zimetengwa na ulimwengu mwingine kimaendeleo.Watu wametumia vigezo vya vyanzo vya utalii kuwanyima wananchi hao maendeleo mbalimbali.Wananchi hawa wametunza mali asili zote hizi bila kuona faida kubwa ya utunzaji huu.Hakuna shirika lililowahi kuja na kujaribu kufanya tathmini ili kuona ni kwa kiasi gani wananchi wale wamenufaika na rasilimali hizo.
Wananchi hawa wamekuwa nyuma kielimu na kimaendeleo na sasa ni wakati muafaka kuruhusu barabara hii iwe kichecheo cha mabadiliko ya maisha ya wananchi wanaozunguka hifadhi hii ya Seregeti.Ni wazi kwamba barabara hii ikisimamiwa vizuri itafungua mianya mingi ya maeondeleo kwa wanachi wa mikoa yote miwili.
Mfano Wananchi wanaoshi Tarafa ya Ngorongoro Wilayani Ngorongoro kwa muda mwingi wamenyimwa kujishugulisha na shughuli zingine za kimaendeleo mbaya zidi hata fedha wanazopata kama mgawo wa mapato ya mamlaka ya Ngorongoro ni ndogo na nyingine huishia kuliwa na wajanja. Kama mtu halimi, hajaenda shule, hafanyi biashara na hana mahala pa kuchungia mifugo , je maisha yake ya baadaye yatakuwaje?
Kwa muda mwingi sasa wananchi wa wilaya za Ngororngoro na Serengeti wamekuwa wakirubiniwa na vipesa vidogovidogo hasa kupitia baadhi ya viongozi wao kuruhusu maeneoa yao yapokonywe.Mfano Loliondo kwa sasa Kampuni ya Thomson Safari inaendelea kujitanua katika ardhi ya vijiji kwa kutumia baadhi ya madiwani waroho wa madaraka na pesa.Wananchi kwa sasa wamechoka na vitendo vya ardhi yao kuporwa na kupewa wawekezaji na kuwafanya wao wakimbizi ndani ya ardhi yao.Mtakumbuka kuwa wananchi wengi walipinga kuwepo kwa makpuni ya OBC na Thomson katika ardhi yao ya malisho.Jitihada hizi zilishia wengi kupigwa risasi na wengine kuishia mikononi mwa polisi.
Mazingira kama haya ndio yanawafanya wanachi sasa wafikirie njia mbadala ya kujikwamua kimaendeleo baada ya kuona hawana tena maeneo makubwa ya ufugaji.Tukumbuke kuwa kwa sasa hali ya ukame ni tishio na pia maeneo makubwa yameshikiliwa na makampuni na hoteli za kitalii wilayani Serengeti na Ngorongoro.
Kuwepo kwa barabara hii itasaidia wanachi wale kubadilika na kujaribu kufanya shughuli zingie za kimaendeleo kama vile biashara.Pia Barabara hii itasaidia kwa kiasi kubwa kufungua soko la mifugo na mazao ya mifugo kama vile ngozi na nyama.


Ndugu msonaji hiyo ndio hali halisi na maoni ya wananchi, Benki ya Dunia pamoja na
TANROAD juu ya barabara ya Musom-Loliondo-Arusha.Soma Toleo la Tano.

By Onesmo Olengurumwa
Vice President Ngorongoro Elites Association NDUSA-ndusa@gmail.com