Wednesday, May 11, 2011

Serengeti High Way -“Kanuni ya Uhuru wa Nchi Kutumia Maliasili Hatarini"



________________________________________
Sehemu ya Kwanza
Mbuga ya Serengeti ambayo inaaminika kuhifadhi aina muhimu ya wanyama Duniani, ilitangazwa kuwa Hifadhi ya Taifa mwaka 1951 na kufanyiwa marekebisho ya mipaka mwaka 1959.Na ifadhi ndogo ya wanyama ya Maswa iliunganishwa na hifadhi ya asili Serengeti-Ngorongoro mwaka 1981. Kupitia Shirika la Kimataifa la Elimu na Utamaduni (UNESCO), Serengeti iliingizwa katika orodha ya Maeneo ya Uridhi wa dunia mwaka 1981.Jamii ya Kimasaai iliyokuwa inaishi katika sehemu kubwa ya wilaya ya Ngorongoro -wakati ule Maasai Province walilazimishwa kuhama maeneo ya serengeti ili kupisha upanuzi wa ifadhi ya serengeti mnamo mwak1959.Sehemu hii ya kwanza ya makala hii imelenga kukuelimisha mambo ya msingi kuhusu uhuru wa mataifa kutumia mali asili bila kuingiliwa(Permanent Sovereignty over natural resources) hasa tunapozungumzia mpango wa serikali wa kuwajengea barabara ya lama ya kuwaunganisha wananchi wa Mikoa ya Mara na Arusha .

Tukumbuke kuwa mpango huu wa kujenga barabara hii ya kutoka Musoma kupitia Loliondo hadi Arusha ulikuwa ni mpango wa Serikali tangu mwaka 1980.Serikali ya Raisi Nyerere kipindi kile ilishindwa kutekeleza mradi huu kutokana shinikizo la wakubwa toka nje.Mpango huu ulipata pigo la kwanza na kuiacha serikali ikiduwaa toka kwa Benki ya Dunia miaka 20 iliyopita.Benki hii ya dunia ilitumia uwezo wake wa kifedha kuishinikiza serikali ya Tanzania kuacha mara mmoja mpango wa barabara hiyo.Cha kushangaza zaidi Benki ya Dunia ilitumia repoti yake ya tathimini ya mazingira kuhalalisha hoja yao ya kuzuia maendeleo kwa watanzania kwa watanzania wa mikoa hiyo miwili.Kwa miaka mingi sasa ukoloni wa kileo umekuwa ukitumia fursa mbalimabali kutenganisha kati ya uhifadhi mazingira na malenngo ya maendeleo ya jamii.Wanaharakati wengi wanaotetea maslahi yao katika suala la mazingira walitumia nafasi hii pia kupokonya uhuru wa Tanzania kupanga mipango yake ya maendeleo.



Mara tu baada ya kushika hatamu ya uongozi wa serikali awamu ya nne waziri mkuu mstaafu Edward Lowassa na raisi Kikwete walilibua upya , tena kwa uzalendo mkubwa mpango huu wa barabara ya Musoma-Arusha. Lengo kubwa la kuwepo kwa barabara hii ni kuunganisha wilaya za Serengeti, Musoma na Loliondo kwenye mkondo wa barabara za kitaifa.Mpango huu wa barabara Musoma –Arusha kupitia Loliondo ni mpango ambao upo kwenye mpango wa miaka kumi ya maendeleo ya barabara nchini.Mwaka 2010 Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzaia ilidhinisha mpango huu rasmi kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Musoma –Arusha yenye gharama ya dola za kimarekani millioni $480 ambazo ni sawa ni bilioni 648,000,000,000/=.

Kama kawaida, mpango huu wa serikali wa kuwaletea wananchi wake maendeleo yao kwa kuwajengea barabara unaendelea kupata shambulizi toka kwa mataifa mbali mbali, mashirika ya kimataifa yanayojiita watetezi wa mazingira, watu binafsi pamoja na baadhi ya mashirika yasiyo ya kiserkali yanafanya kazi hapa nchini.Cha kusikitisha zaidi, baadhi ya haya makampuni kama vile kampuni ya Frankfurt Zoological Society yamekuwa yakifanya kazi zao kwa muda mrefu hapa nchini.Serikali yetu imekuwa ikiwakumbatia wawekezaji hawa pasipokujua kuwa leo wangekuja kutunushia serikali yetu misuli pale inapopanga mipango yake ya maendeleo.


Baadhi ya wahafidhina hao wanaoping maendeleo ya jamii walienda mbali na kutamka kuwa serengeti ipo chini ya UNESCO , hivyo Tanzania haina uwezo wa kufanya chochote.Suala hili liliuchoma moyo wangu na kuamua kuzungumza kupitia makala hii.

Wapendwa wasomaji na wananchi watiifu wa Tanzania, naomba awali ya yote katika sehemu hii ya kwanza nitumia fursa hii kuwaelimisha juu ya mambo kadhaa kuhusu uridhi wa dunia na uhuru wa nchi kutumia rasilimali zake.Urithi wa kiutamaduni ni jumuiko la vitu vyeye thamani ya kidunia kutokana na historia, sanaa au sayansi; baadhi ya vitu hivi ni pamoja masalio ya vitu vya kale, kazi za sanaa,majengo, maandishi na mapango. Mifano ya uridhi huu hapa Tanzania ni: Mji Mkongwe,Majengo ya Kilwa na Mnara wa Songo.Uridhi wa mali asili unamaanisha vitu vyote vya kiasilia vyenye thamani kidunia na vilivyotekea kutokana na mfumo na mabadiliko dunia ya kimaumbile na kibaiolojia.Mifano ya mali asili hii hapa Tanzania ni: Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro, Hifadhi ya Serengeti, Hifadhi ndogo ya Selou na Hifadhi ya Ngorongoro.

Uhuru kwa mtazamo huu inamaanisha uwezo wa nchi yoyote ile kujitawala na kutengeza sheria na mipango yake ya maendeleo bila kushurutishwa au kuingiliwa na chombo chochote au nchi nyingine.Uhuru wa nchi juu ya rasilimali zake unamaanisha kuwa inchi inahaki ya kutumia rasilimali zake bila kuingiliwa au kushurutishwa.Kwa kutambua haki hii kwa mataifa, mazimizio kadhaa ya kusisitiza haki hii yalipitishwa miaka ya 1960 na Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa.Umoja wa Mataifa walitambua haki hii kama haki muhimu kwa nchi yoyote ile kijitawala.Na hatimaye Umoja wa Mataifa walipitisha azimio numba 1803 (xvii) mwaka 1962 ili kuipa nguvu haki hii katika nyanja ya kimataifa.Mkutano huo wa Kimataifa ulikubaliana kama ifuatavyo;
“Haki ya mataifa na watu kuwa huru kutumia rasilimali zao na utajiri wao lazima utekelezwe kwa kuzingatia maslahi ya maendeleo yao na ustawi wa wananchi wa mataifa husika”

Azimio hili la Umoja wa Kimataifa katika nyanja hii iliweza kuwa chachu katika mikutano mingi ya kimataifa. Mfano, mwaka 1966 kanuni hii ya uhuru wa rasilimali iliingizwa rasmi katika mikataba mbali mbali ya kimataifa ikiwemo mkataba ule wa Haki za Kiuchumi, Kijamii na Kitamaduni wa mwaka 1966. Kuanzia miaka ya 1960 Umoja wa Kimataifa ulipitisha zaidi ya maazimio 100 yanayotetea utekelezaji wa kanuni hii ya huru wa rasilimali.Mfano, kanuni ya 21 ya Azimio la Stokholm la mwaka 1972 unasisitiza kuwa:
“Mataifa kwa mujibu wa Mkataba wa Umoja Kimataifa na kanuni za sheria za kimataifa yana haki na uhuru wa kutumia rasilimali zao bila kuingiliwa, na kutumia na kusimamia rasilimali hizo kwa mijibu wa sheria zao na kuhakikisha shughuli zao haziwezi kuleta madhara yoyote kwa mazingira ya nchi zingine au maeneo nje ya mipaka yao”
Kifungu cha 4 cha Mkataba wa UNESCO wa mwaka 1972, unaeleza kuwa jukumu la uhifadhi wa mazingira na uhifadhi wa uridhi wa maliasili na uridhi wa kiutamaduni kwa vizazi vijavyo ni la nchi husika, lakini kwa hiari nchi husika inaweza kuomba msaada kutoka ushirika wa kimataifa na wakapata.
Halikadhalika, mataifa yanatakiwa kufuata masharti yote ya Mkataba wa UNESCO.Tatizo kubwa la makataba huu ni lile la kutambua Uridhi wote wa dunia kama uridhi wa dunia na ni lazima uridhi huo utunzwe kwa manufaa ya wote duniani.
Mkutano wa Umoja wa Kimataifa wa Stokholm wa 1972 wa watu na mazingira, ulikuja na azimio lenye kanuni 26 za sheria za kimataifa za mazingira .Uhusiano kati ya binadamu na mazingira umewekwa bayana katika kanuni ya 1,16 na 21 vya azimio hilo.Kanuni hizo zinasisitiza uhuru wa mataifa kutumia rasilimali zao bila kuharibu mazingira na pia bila kuvunja haki yoyote ya binadamu.
Utekelezeja wa mkataba huu wa UNESCO mara nyingi utekelezaji wake umekuwa ukivunja haki hii ya msingi ya mataifa kutumia rasilimali kwa maslahi ya taifa husika.Hili linawezekana kutokana na kwamba sehemu yoyote ya nchi ikitangazwa kuingia katika orodha wa vitu ambavyo ni uridhi wa dunia, eneo hilo linakuwa ni rasilimali ya wote na pengine nchi husika kama itakuwa legelege huenda ikapoteza uhuru wa kusimamia eneo hilo kwa mijibu wa sheria na mipango yake.
Baada ya eneo kutangazwa huwa chini ya sheria za kimataifa na sheria za nchi., lakini sheria zetu mara nyingi zimekuwa zikizidiwa kutokana na ukandamizaji na jeuri ya fedha za wakubwa.Mfano wa maeneo ambayo nchi kwa sasa inapelekea kukosa uhuru wa kufanya inaloona ni sahihi kwa maslahi ya umma ni Hifadhi ya Ngorongoro na Serengeti.Mapema mwaka 2009, UNESCO ilitishia kuitoa Bonde la Ngorongoro kwenye orodha ya uridhi wa dunia kama haitafuata masharti yao. Il kuwaridhisha, Naibu Waziri Maliasili wa wakati ule Mh.Ezekiel Maige alisikia askisema:
“Tayari tumeshaanza kutoa majukumu kwa wahusika kujua idadi ya watu na mifugo kaika eneo hilo ili tuweze kuchukua hatua zinazostahili.”
Hii inadhirisha kuwa mkataba wa UNESCO inakinzana na kanuni ya uhuru wa rasilimali.Mbaya zaidi vifungu vya mkataba wa UNESCO kwa sasa unatumika na baadhi ya taasisi za kizushi na zisizojulikana pamoja na wachache wennye njaa kupinga mpango wa serikali kujenga barabara ya Musoma hadi Arusha kupitia Loliondo. Lakini katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 9 inasisitiza kuwa:
“Kama suala la kisera , rasilimali zote za nchi zitatumika kuleta maendeleo ya watu na hasa kupunguza umasikini, ujinga na maradhi, huku utu wa binadamu ukizingatiwa na kulindwa kama inavyoelezwa na Azimio la Kimataifa la Haki za Binadamu”
Pia katiba ya Tanzania inaweka bayana kuwa rasilimali za nchi za nchi zitumike kupunguza umasikini bila kuangalia kabila, dini, umri au eneo analo ishi mtu.Hivyo ni kinyume na katiba kuishinikiza serikali kupeleka miradi ya maendeleo kama mradi huu wa barabara upande mmoja wa nchi kwa vigezo vya ulinzi wa mazingira au kigezo cha uchache wa watu.Sababu nyingi zilizotolea na wanaopinga miradi ya serikali hazikubaliki, zipo kinyume na katiba, hazina hoja ya msingi, ni za kizushi na zinakiuka misingi ya haki za binadamu.Sababu hizi zinatokana na ubinafsi na uchu wa fedha wa baadhi ya watu wanaotumia na wakubwa hawa wanaoendeleza ukoloni wa kileo katika nyanja ya mali asili.
Nchi zingine zilifikia hatua kuanzisha siku ya serengeti duniani na kuazimisha katika nchi zao.Mwaka huu siku ya serengeti duniani ili anzimishwa sehemu mbalimbali duniani lakini Tanzania ambayo ndiyo yenye serengeti yenyewe ilikuwa kama vile haijui chochote kinachoendelea. Mfano, nchi jirani ya Kenya waliazimisha siku ya serengeti duniani mwaka huu machi katika viwanja wa Uhuru Park Nairobi huku wakishinikiza barabara ya Musoma Arusha isijengwe.Ndugu wasomaji, je huko sio kuingiliana katika mambo ya ndani ya nchi?
Kama tutaruhusu utawala wa dunia juu ya rasilimali zetu, hakika wananchi hawatakuwa na cha kujivunia.Hali inayoikumba Tanzania kwa sasa iliwahi tokea Wyoming mwaka 1995 dhidi ya Yellow Stone Park pale ambapo kamati ya uridhi wa dunia ya UNESCO kutoka Ulaya waliungana na wanaharakati wa uchwara wa mazingira kupinga shughuli za uchimbaji zilizokuwa zikifanyika Wyoming. Hali kama hii ya utegemezi wa misaada ya kimataifa imegeuka kuwa dhana ya kugandamiza na kupora uhuru wa rasilimali kwa nchi nyingi zinazoendelea.Tanzania kwa miaka mingi imekuwa ikitishiwa na wahisani na mataifa makubwa hasa pale inapopanga mipango yake ya maendeleo kama hili la barabara ya Musoma kwenda Arusha.Mbaya zaidi kifungu cha 26 cha Mkataba wa UNESCO unasisitiza kuwa:

Lakini imekuwa kutambua nini kitakuwa ndani ya makubaliano hayo na uhuru wa nchi husika.Hili linapelekea kuhamisha uhuru wa nchi kusimamia rasilimali zake kwenda kwenye mamlaka ya kimataifa.Katika hali ya utegemezi na misaada wa kimataifa nchi nyingi zinapoteza uhuru juu ya rasilimali za ndani.
Ili kupata maendeleo ya usawa , yanayokizi maslahi ya kimazingira na maendeleo ya watu , ni muhimu mataifa yakawa na utaratibu shirikishi, huru na wa wazi katika mipango ya maendeleo ili kuhakikisha mipango ya utunzaji wa mazingira yanakwenda samba samba na uhitaji wa kuboresha maisha ya wananchi.Hivyo nchi zilizoendelea ziache kuendeshwa na wanaharaki wanaozuka na kujiita watetezi wa mazingira.Pia waache kutumia utajiri wao kuingiliia mambo ya ndani ya nchi.Tunaishauri serikali iendelee na mpango wake wa kujenga barabara ya Musoma –Arusha maana Tanzania ni nchi huru.
By Onesmo Olengurumwa
Makamu wa Raisi Umoja wa Wasomi Ngorongoro- NDUSA
ndusa@gmail.com

1 comment:

Masegeri said...

Nakupongeza kijana kwa kutoa ufafanuzi mzuri na mawazo yenye uzalendo.Kimsingi ni kwamba hizi nchi zilizoendelea zinapigania maeneo kama serengeti ili waananchi waweze kuwa na maeneo ya kwenda kustarehe wala hakuna cha kusema eti wanajalai au kuetetea mazingira.Wangekuwa wanajali mazingira wangeacha kutumia fedha zao nyingi walizozipa kwa njia ya Ukoloni kwa mambo ya anasa na badala yake wangesaidia watu kwenye nchi maskini kuboresha maisha yao.Lakin pia nchi kama marekan ambayo ni namba moja kwa kuzalisha gesi ukaa( CO2) dunian imekataa kusaini mkataba wa Kyoto unaozitakanchi tajiri kupunguza viwanda vyao vinavyozalisha gesi hiyo.Kwaiyo hakuna dhamira ya ukweli ya kuhifadhi mazingira ila suala mazingira limekuwa ni sehemu ya Ukoloni mamboleo na silaha ya kuziganadamiza nchi maskini.Tuombe serikali yetu isimame imara ili isiyumbishwe na hawa mabwenyenye.