Sunday, January 16, 2011

MA DC NA RC WAGEUKA MIUNGU WATU

WAKUU MIKOA/WILAYA WAGEUKA MIUNGU WATU
Uongozi bora ni uongozi unaoheshimu utawala wa sheria na haki za msingi za raia. Uongozi bora ni lazima utambuliwe kwa kuangalia ni kwa jinsi gani viongozi wetu wa ngazi zote wanatumia madaraka yao vizuri bila kuingilia uhuru wa vyombo vingine vya dola. Kila chombo kinachounda dola ya nchi ni lazima kifanye kazi kwa kuzingatia mipaka yake na kueshimu majukumu ya dola nyingine. Serikali ni mojawapo ya mihili miwili ya dola tuliyonayo hapa Tanzania. Ili kusema nchi inatawaliwa kidemokrasia na kwa kuzingatia vyombo vya dola, ni lazima kuwepo na serikali tiifu, yenye kuheshimu haki za raia na yenye kufuata matakwa ya watawaliwa.
Serikali ya Tanzania imegawanyika katika makundi mawili: Ngazi ya kwanza ni Serikali Kuu na ya pili ni Serikali za Mitaa. Serikali kuu inajumiusha utawala wa mikoa na Wilaya. Wakuu wa mikoa na Wilaya ndio watendaji wakuu wa serikali kuu mikoani wakimwakilisha Rais wa nchi. Hawa wote hupatatikana kwa njia ya kuteuliwa na Rais wakishirikiana na Waziri Mkuu. Wakuu hawa pia ndio wenyeviti wa kamati za ulinzi na usalama wa mkoa na wilaya, na pia ndio wenyeviti wa kamati za siasa kupitia chama Tawala.
Hivi karibuni Wakuu wa wilaya na mikoa wameonyesha utendaji usiokuwa na sura ya uongozi bora. Viongozi hawa wamekuwa wakitumia madaraka yao vibaya kwa kufanya maamuzi yasiofuata misingi ya utawala wa sheria. Matuikio mengine yameonyesha viongozi hawa wakiingilia uhuru wa wa utendaji wa vyombo huru vilioundwa na bunge, mfano tarehe 16 April,2010 Mkuu wa mkoa wa Kigoma aliamuru kufungwa na kumtoa nje ya ofisi mwenyekiti wa Baraza la Ardhi na Nyumba wa Kigoma. Baraza la ardhi na Nyumba ni Mahakama huru iliyoundwa kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi ya mwaka 1999 kifungu cha 167 na kifungu 22 cha Sheria ya Mahakama ya Migogoro ya Ardhi ya 2002.
Pia Wakuu wa wilaya wameonekana mara kwa mara wakiingilia Uhuru wa vyombo vya habari kwa kuwatishia na hata kuwatia mbaroni baadhi ya waandishi wa habari wanaojaribu kufichua maovu yanayotendeka katika jamii. Mwaka huu waandishi wa habari watatu walitiwa mbaroni kwa amri ya mkuu wa wilaya wa Hanang kwa kudaiwa kuwa wamekuwa wakiitisha vikao vya uchochezi. Waandishi wa habari wengine pia katika sakata la Loliondo walizuiwa kufuatilia maandamano ya Kina mama kwa kutakiwa kujitambulisha kwa mkuu wa wilaya kabla ya kuanza shungulizi zao za ukusanyaji wa habari. Pia tarehe 5 May,2010 Mwandishi wa habari wa televisheni ya ITV Cosmas Makongo pamoja na mpiga picha wa ITV walifukuzwa na kuwekwa chini ya ulinzi wa polisi baada ya Mkuu wa wilaya ya Ngara Kuamuru waandishi wa habari wasihudhurie mkutano huo wa hadhara na baadaye kuhojiwa na maafisa wa uhamiaji. Vitendo hivi vinavyofanywa na wakuu wa wilaya hukiuka kifungu cha 18 cha katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tazania, kinachotoa haki ya Kutoa maoni , kukusanya nakupata taarifa bila masharti yoyote.
Viongozi hao pia wamekuwa wakitumia madaraka yao kuua dhana ya uwazi na ukweli kwa maslahi yao binafsi. Kwa Mujibu wa Kifungu cha 18 (d) Kila Mtanzania ana haki ya kujulishwa na kupata taarifa kuhusu mambo ya msingi yahusuyo maisha yake ya kila siku. Hivi karibuni Mkuu wa wilaya ya Hanang aliamuru viongozi wawili wa kijiji cha Masquoroda kutiwa mbaroni kwa sababu viongozi hao walitaka mchanganuo wa matumizi ya pesa za mwenge walizochanga kabla ya kuanza michango mingine ya mwaka huu. Vile vile katika Mkoa huo huo wa Manyara wanachi walionekana wakinyimwa haki yao ya kuhoji kwa kutakiwa kutoka nje ya kikao, suala lililopelekea ugomvi mkubwa kati ya Mbunge wa Simanjiro mtetezi wa wananchi na Mkuu wa Mkoa wa Manyara.
Pamoja na hayo hivi karibuni wakuu wa mikoa na wilaya wamekuwa wakishutumu, kutishia na kutupia lawama asasi za kiraia zinazotetea haki za wanyonge Tanzania. Mfano, wawakilishi watatu wa asasi za kiraia zinazofanya kazi wilayani Ngorongoro waliwekwa rumande na kunyimwa dhamana kwa muda wa siku moja kwa madai ya kwamba wao ndio waanzilishi wa maandamano ya akina mama yaliyotarajiwa kufanyika Loliondo mwezi April,2010. Waliokamatwa ni wafanyakazi wa mashirika yasiyo ya kiserikali yanayotambulika Kisheria kwa kuwa na usajili sahihi kwa mujibu wa Sheria ya mashirika yasiyo ya kiserikali nambari 4 ya mwaka 2002. Hivyo basi, viongozi wa usalama Wilayani Ngorongoro walipaswa kufuata taratibu kwa mujibu wa sheria hiyo.Huko Songea DC Ole Sabaya kageuka tishio kwa NGOs na wafuasi wa vyama vya upinzani.
Wanaharakati tumebaini kuwa baadhi ya viongozi wa serikali mikoani hasa wakuu wa mikoa na wilaya wamegeuka kuwa miungu watu kwa kutumia madaraka yao vibaya bila kujali dhana nzima ya utawala wa sheria. Ili Tanzania ijitambulishe kama nchi inayo ongozwa kwa misingi ya utawala bora, watanzania wote tunapaswa kukemea vitendo vyote viovu vinavyofanywa na watawala wetu mikoani. Viongozi wa mikoa na wilaya wanapaswa kuwa wawajibikaji, wawazi na wenye kuheshimu haki za msingi za binadamu kama zilivoainishwa katika katiba ya Nchi.

No comments: