SEHEMU YA TANO
Mpendwa Msomaji, baada ya kusoma toleo la nne na kuweza kuona misimamo ya viongozi wa Kitaifa kuhusiana na sakata hili la barabara.Makala hii inakuletea msimamo wa Wizara ya Maliasili kuhusiana na ujenzi wa barabara ya kuu ya kutoka Arusha hado Musoma kupitia Loliondo.Hivi karibuni Waziri wa Maliasili Ezekiel Maige alimwandikia barua ya msimamo wa Wizara, Mkurugenzi wa Shirika la Utamaduni na Maliasili Duniani(UNESCO).Barua hiyo ya tarehe 22/5/2011 ni kama vile ilikuwa inajibu matakwa ya UNESCO. Kichwa cha Habari hiyo inajibu malalamiko na vitisho vya UNESCO na mataifa tajiri dhidi ya mpango wa serikali ya kujenga barabara kwa watu wake.
Barua hiyo inaelezea jinsi serikali ilivyoshindwa kusimamia msimamo wake wa kujenga barabara kuu ya kuwaunganisha watu wa kanda ya ziwa na mikoa ya Kasakazini kiuchumi. Hapo awali malengo ya Serikali yalikuwa ni kuwaunganisha wanachi wa mikoa hiyo kiuchumi. Lakini kwa mujibu wa barua ya Waziri Ezekiel Maige kwa UNESCO mpango huo umekufa kifo cha taratibu wanachi wamepumbazwa kuhusiana na hili.Ukweli ni kwamba mpango wa serikali wa kujenga barabara toka Musoma hadi Arusha kupitia Loliondo haupo tena na badala yake kitakachotekelezwa na mipangao ya UNESCO, Frank Foot Zoological Society, WB na Nchi kama Ujerumani na Kenya.Njia ya kaskazini(Nothern route) ndugu watanzania haupo tena na kinachofanyika sasa ni kujenga barabara za wilaya 3 Serengeti, Monduli na Ngorongoro.Najaribu kuitafsiri barua hiyo kama ifuatavyo; Mpango wa barabara kwa sasa umegawanyika mara mbili, ukanda wa mashariki ambao upo ndani ya Ngorongoro barabara itajengwa kwa kiwango cha lami toka Mtoambu hadi Loliondo kupitia Ziwa Natron kwa urefu wa kilometa 214 , upande wa mashariki ambao upo wilayani Serengeti watajenga kilometa 117 toka Makutano-Natta-Mugumu na sehemu ya katikati toka Mugumu hadi Loliondo kama umbali wa kilometa 100 haitajengwa kwa kiwango cha lami.
Kwa uchambuzi wa harakaraka ni kwamba serikali imezidiwa kete na mataifa makubwa.Je ule mpango wa kuwaunganisha watanzania wa kanda ya ziwa na wa kaskazini bado upo? La hasha haupo tena, mkubwa akipigwa halii, serikali haitaki kusema ukweli.Iweje leo waseme zile kilometa 53 zitabaki chini ya Usimamizi wa TANAPA.Je Loliondo hadi Lolosokwani ipo chini ya Tanapa.Je barabara hizi tutaziita tena High way-Njia kuu? la hasha ni barabara za ndani za wilaya na huu ndio mpango uliokuwa wa Nchi kama ya Ujerumani.
Ule mpango wa kiuchumi sasa umekufa, barabara kwa sasa itawasaidia tu wanachi wa wilaya zile kwenda Arusha Mjini kirahi lakini sio kufungua fursa nyingi za kiuchumi.Mpango huu unaweza kuwa umeleta ushindi sawa ( Win win situation) kama wengine wanavyosema.Wanaojiita Watetezi wa maliasili watakuwa wameshinda zaidi na ndio maana wengine wamejitangaza wameshinda vita vya serengeti.Nasema hakuna fursa sawa kutokana na kwamba bado wale wananchi wa wilaya zile wataendelea kubaki wenyewe bila muunganiko wowote.Na pia haiwezi kuwa win win situation(fursa sawa) kwa sababu yale malengo ya serikali ya kujenga barabara kuu (High way) yametoweka.
Kwangu mimi binafsi naona ni udhaifu mkubwa kwa serikali ya nchi huru kama Tanzania.Hapa kuna tatizo la kuongozwa na mataifa makubwa katika mambo ya msingi ya Taifa letu.Hii hatuwezi sema kuwa ni win win sutuation ilhali uhuru wa Taifa letu unachezewa.Maamuzi ya Taifa letu yanapaswa kutekelezwa bila kuingiliwa na Taifa au Shirika lolote.Tabia hii ikizoeleka hakika tutukuwa taifa mfu ambalo kila tunalolipanga tunahitaji kupewa ruksa au laa na mataifa makubwa na wakati mwingine mashirika ya kimataifa.Ugonjwa huu tunatakiwa tuukemee kwa nguvu zote.
Mwishoni wa Aprili mwaka huu Mkurugenzi wa Benki ya Dunia wa nchi za Africa Mashariki, pamoja na viongozi wengine wa serikali walikuwa eneo la Loliondo hasa kata ya Soit na kuwaahidi wanachi wale kuwa barabara itajengwa.Sasa inakuwaje leo barua ya waziri wa maliasili ikinzane na watu wa TANROAD. Je barua ya Waziri Maige ni Msimamo wa Serikali au wizara? Tukumbuke kuwa ujenzi wa barabara upo nchini ya Wizara ya Ujenzi kitengo cha wakala wa barabara (TANROAD). Hata hivyo taarifa zingine zinaonyesha kuna watu katika wizara hizi mbili hawaungi mkono hoja ya serikali kuwa na barabara kuu inayowaunganisha wanachi wa kanda ya Ziwa na wananchi wa mikoa ya kaskazini kiuchumi.Hii ni changamoto kwa ustawi wa nchi kama hizi ambazo ni changa kiuchumi.Watu wote wanapaswa kuwa wazalendo pale serikali inapokuwa na mipango ya kuinua watu kiuchumi.Mipango ya maendeleo haipaswi kupingwa kabisa bali kusahishwa.Mfano mipango kama MKUKUTA wengi hatuupingi bali tunakosoa na kutoa mawazo nini kifanyike mafanikio ya kweli yaonekane.
Hivi karibu mikutano mingi ya UNESCO imefanyika na suala ya barabara ya Musoma –Arusha ilikuwa gumzo.Pia baadhi ya viongozi wetu toka wizara ya Ujenzi wamekwenda Ujerumani kueleza msimamo wa serikali kuhusu barabara hiyo.Je wamekwenda kutoa ufafanuzi au kusihi Ujeruman wakubali mpango wa barabara.Tatizo la umaskini limekuwa chanzo kikubwa cha nchi za ulimwengu wa tatu kutokuwa na uhuru wa kijiamualia mambo yake ya msingi.Kutokana na ukweli kwamba fedha zitatoka kwa hao hao wanaopinga mpango wa serikali. Tusubiri kwa hamu nini kilichojiri huko Ujerumani.
Nadhani inafika mahala nchi hizi zifikirie namna ya kujikwamua kiuchumi ili kuondokana na utegemezi unaotudhalilisha. Nchi hizi omba omba kama Tanzania hakika hatuwezi kufanya lolote kinyume na matakwa ya wahisani.Ni ukweli usiopingika kuwa hatuko huru kiuchumi na hasa upande wa mali asili.Na ili tuepukane na hili pia nchi inaweza kutumia nchi zingine kama China, Japan, Russia na Korea kuondesha miradi mingine ya kimaendeleo na sio tu nchi za magharibi. Mimi naamini zipo nchi nyingine zingeweza kujenga barabara hapa nchini bilaa kuleta masharti magumu.
Hivyo ndoto ile ya kufanya mikoa ya kanda ya ziwa kuwa pamoja kiuchumi na mikoa ya kaskazini na kwa kupitia barabara kuu ya Musoma- Arusha kupitia Loliondo sasa haipo tena.Kuwepo kwa barabara ile ingeuwa soko la Nairobi na wilaya za Kenya jirani na Tanzania ambapo kwa sasa ndio hutumika zaidi na wanachi wa mipakani.Pengine ndio maana Kenya ndio nchi pekee ya Africa Mashariki iliyoonekana kupinga mpango wa barabara hii.
Na Onesmo Olengurumwa-Mtafiti na Mwansheria LHRC, Pia ni Makamu wa Rais Mtandao wasomi Ngorongoro.Opngurumwa@gmail.com
No comments:
Post a Comment