Wafugaji ni wavamizi warudi walikotoka?Je kauli hizi ni saw?
Mussa Juma.
KATIKA siku za hivi karibuni, wafugaji wamekuwa wakiondolewa maeneo mbalimbali nchini, kwa kuitwa wavamizi na kutakiwa warudi walikotoka.
Kauli za kuwafukuza wafugaji hawa, zimekuwa zikitolewa na viongozi wa ngazi za juu serikani hadi wa za chini hali ambayo imekuwa ikizua migogoro katika maeneo mengi.
Matamko ya viongozi hawa yanatokana na ukweli kuwa wafugaji kutoka mikoa ya kanda ya kaskazini na ziwa wamesambaa katika maeneo mengi nchini kusaka malisho. Wafugaji wa Kimasai, Kibarbeig na Kisukuma ndiyo ambao kwa kiasi kikubwa wamekuwa wakifukuzwa katika maeneo mengi kwa maelezo kuwa ni wavamizi.
Baadhi ya maeneo ambayo wafugaji hao wanafukuzwa kwa kuitwa wavamizi na kutakiwa kurudi walikotoka ni Kilosa, Mvomero mkoani Morogoro, Bunda mkoani Mara, Bagamoyo mkoani Pwani, Loliondo mkoani Arusha na maeneo ya Mikoa ya Rukwa na Iringa.
Hata hivyo, wakati wafugaji hawa wakifukuzwa kila eneo wanalokwenda bado hakuna utafiti wa kina ambao umefanywa na serikali na kubaini chanzo cha kuhama katika maeneo yao ya asili.
Nahisi haitaki kuwa wazi juu ya walikotoka, inajua kuwa ndiyo iliyowaondoa katika maeneo yao.
Kwa mfano, kuanzia mwaka 1959, wafugaji wa Kimasai walianza kuondolewa katika maeneo yao Serengeti ilipoanzishwa na kuwa Hifadhi ya Taifa baadaye. Wafugaji wa Kibargeig nao waliondolewa wilayani Hanang' miaka ya 1970 na kuanzishwa mashamba makubwa ya lililokuwa Shirika la Taifa la Kilimo (Tafco).
Haikuishia hapo, miaka iliyofuata wafugaji wa Kisukuma waliondolewa maeneo ya Maswa kupisha kuanzishwa kwa pori la akiba. Pia wafugaji waliondolewa Same na Mwanga na kuanzishwa Hifadhi ya Mkomazi.
Wafugaji hawa pia waliondolewa maeneo ya Tarangire, Manyara, Ruaha na kuanzisha pia Hifadhi za Taifa na kihistoria maeneo yote haya ambayo sasa yana wanyama yalikuwa ya wafugaji.
Licha ya kuanzisha hifadhi, pia upanuzi wa mashamba makubwa na ongezeko la watu kwenye maeneo mengi nchini, kumechangia kuwasukuma wafugaji kutoka katika maeneo yao ya asili ili kusaka malisho. Ufugaji huu wa Tanzania hauna tofauti na ule wa asili wa maeneo mengine duniani, kama Sudan, Ethiopia, Uganda Kenya na nchi nchi za magharibi.
Wafugaji wote wa asili wana tabia zinazofanana, wakati wote hutembea kutafuta malisho na maji na hii inatokana na kutambua kuwa kukaa sehemu moja kunasababisha athari za mazingira.
Wafugaji hata katika maeneo yao ya vijijini wamekuwa na tabia ya kuhamahama ili kuhakikisha wakitoka eneo moja wanapisha majani kuota. Ufugaji wa aina hii upo Wilaya ya Simanjiro ambako kuna maeneo ya Kata kama za Terati, Sukuro, Naberera na nyingine ambazo wafugaji hujipangia wakati wa kwenda kulisha mifugo.
Jambo hili la kuhamahama, limekuwa likitumiwa vibaya na wakulima. Wafugaji wanapohama, wakulima wamekuwa wajikatia ardhi na hata kuimiliki bila kujua desturi na mila za wafugaji wa asili.
Serikali inaweza kumaliza migogoro ya wafugaji na kufuta kauli za viongozi za kuwaita wavamizi, warudi walipotoka au kuwataka wauze mifugo yao kwa nguvu kama ilivyotokea Kilosa na Rukwa. Inaweza kutenga maeneo makubwa ya malisho ya mifugo na kutangaza kuwa ni ya wafugaji wa asili kwa kuyaanzishia ranchi ambazo licha ya kusaidia wafugaji kutohamahama pia itasaidia kubadilisha mifugo yao ya asili.
Maeneo mengi ya wafugaji hayana majosho, mabwawa na hakuna miundombinu ambayo inayoweza kuwafanya wafugaji kuaa bila kuhama. Ni kutokana na kuwekewa mazingira ya kutothaminiwa, wanaendelea kufilisika. Miaka 15 ijayo athari za kauli za kuwaita wafugaji wa asili ni wavamizi na kuwataka warudi walikotoka zitaonekana.
Athari za wazi kabisa ambazo zitawagusa watu wengi ni kupungua kwa nyama katika maeneo mengi nchini na hivyo kupanda bei maradufu. Naamini hii itawaathiri wananchi wa kawaida.
Viongozi waliopewa dhamana katika sekta ya mifugo wanapaswa kuacha kuhubiri siasa na badala yake waanzishe mkakati kuwasaidia wafugaji popote walipo ili wafuge kisasa badala ya kuwafukuza.
Madhara ya kutothaminiwa wafugaji yapo wazi. Hivi karibini tumeshuhudia mamia ya mifugo ikipotea wilayani Kilosa, makazi ya wafugaji yakiteketezwa kwa moto Loliondo huku maelfu ya mifugo ikiondolewa.
Wilayani Bunda kuna operesheni inayoendelea kuwaondoa wafugaji ambayo sasa imefikia hatua ya kutisha, kwa watoto wadogo wa wafugaji kufungwa kwa tuhuma za kuingiza mifugo eneo la pori.
Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Chiku Gallawa naye amejiunga na kauli za viongozi wenzake kuwa kuna wafugaji wavamizi Bunda na sasa lazima waondoke. Kauli hii ya hivi karibuni inapingana na ukweli kuwa ukame uliopo sasa na kuanzishwa kwa pori la akiba la Grumet na kuwepo Hifadhi ya Serengeti katika wilaya hiyo kumepokonya maeneo mengi ya wafugaji.
Tuanze sasa kuwasaidia wafugaji ili waweze kufuga kisasa, kauli za kuwafukuza kila mahali wanapohamia na kuwataka warudi walikotoka si sahihi. Hivi wakiamua kurudi Serengeti, Maswa, Grumet, Ngorongoro na Hanang nani atawadhibiti?
Mussa ninaungana nawe moja kwa moja.
0754 296503 Email mussasiwa@gmail.com.
Tuma maoni kwa Mhariri
No comments:
Post a Comment