Katiba ni ujenzi wa msingi ambao serikali na sheria
hujengwa juu yake na vile vile ni utaratibu ambao wenye inchi wanatakiwa kuamua
namna ya kuendesha mambo ya msingi katika nchi yao.
Watanzania
mtakumbuka kuwa nchi yetu kwa sasa ipo
katika mchakato wa kutengeneza katiba mpya. Mchakato wa kutengeneza katiba ni
mchakato mpana na unaohitaji kushirikisha makundi yote katika jamii. Makundi
haya yanaweza kushirikishwa katika nafasi na awamu mbalimbali za utengenezaji
wa katiba. Mchakato wa kutengeneza katiba mpya katika nchi yetu umeanzia katika
hatua ya kuwa, kwanza na sheria ya
kutengeneza katiba mpya ambayo tayari kimakosa wameibatiza kwa jina Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba ya Mwaka 2011. Pamoja na makosa yake sehemu ya tatu ya
sheria hii inatoa mamlaka kwa Rais wa Nchi kuunda Tume ya Uundaji wa Katiba
Mpya. Sehemu ya Tano inasema, Rais, baada
ya kushauriana na kukubaliana na Rais wa Zanzibar, na kwa kuzingatia hali ya
kijamii, kisiasa na kiuchumi iliyopo katika Jamhuri ya Muungano kwa amri
itakayochapishwa katika Gazeti la Serikali, ataunda Tume.
Hivi
karibuni Rais Kikwete alipokea majina toka makundi mbalimbali kwa ajili ya
kufanya uteuzi wa Tume ya Katiba yenye wajumbe 32. Uteuzi huu ulipaswa
kuangalia makundi mbalimbali ili kuweza kuwa sehemu ya Tume. Kimsingi ili Tume
hii iweze kuja na rasimu nzuri ya katiba itakayotumika miaka mia moja ijayo na
inayokidhi haja za makundi yote ya kijamii, Rais alipaswa kuzingatia sheria na
kutoa kipaumbele kwa yale makundi ambayo hayana fursa nyingine kubwa ya
kushiriki katika mchakato mwingine wa katiba.Mchakato wa katiba umeganyika
katika awamu mbalimbali ukianzia huu wa Sheria ya Katiba, Tume na Baadaye Bunge
la Katiba. Inakuwa si busara watu wale wale wakashiriki kuongoza michako yote hiyo mitatu. Mfano
wabunge wasipodhibitiwa na sheria wanaweza kuhodhi mchakato mzima na kuwafanya
watu wengine waishie tu kutoa maoni.
Katika
Sehemu ya 5 ya Sheria ya Kuunda Katiba mpya kabla ya kufanyiwa marekebisho
mapema mwaka huu kuna baadhi ya makundi ya watu hasa viongozi wa siasa walikatazwa
na sheria kuwa sehemu ya Tume. Sheria hii ilisisitiza kuwa mtu hatakuwa na sifa
za kuteuliwa kuwa mjumbe wa Tume endapo mtu huyo:
|
a)
ni
Mbunge, Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar, diwani
au kiongozi wa chama
cha katika ngazi zote;
|
b)
ni mtumishi katika vyombo
vya usalama;
|
c)
ni mtu aliyewahi kuhukumiwa
kwa kutenda kosa, au ni mtuhumiwa
katika shauri
lililopo mahakamani linalohusu shitaka la kukosa uaminifu au maadili;
au
|
d)
si
raia wa Tanzania.
|
Katika majadiliano
yaliyofanyika bungeni juu ya mabadiliko
sheria hii miongoni mwa mambo yaliyozingatiwa ni pamoja na kutaka kuwazuia
wabunge na wawakilishi wa baraza la Zanzibar kuwa wajumbe wa bodi. Mhe Angellah
J. Kairuki makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba na Sheria Bungeni alikunukuliwa Bungeni akisema, Serikali
ilikubali kufanya marekebisho zaidi kwenye kifungu hicho ili kizuizi kiwe kwa
Mbunge na Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar kama inavykuwainaonekana
kwenye jedwali la Marekebisho ya Sheria hii. Kabla ya kutoka kwa sheria iliyofanyiwa
mabadiliko na kwa mujibu wa majadiliano ya bunge ilikuwa ni wazi kuwa wabunge na wawakilishi
walizuiwa kuwa wajumbe wa tume.Mhe Kairuki alisem;
“Mheshimiwa Spika, Kamati inakubaliana na mapendekezo ya
Serikali ya kuondoa maneno “au Kiongozi wa Chama cha Siasa wa ngazi zote”
kutoka katika Kifungu cha 6(5)(a) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba (Namba 8)
ya Mwaka 2011. Kamati ilielezwa na Serikali kwamba, mabadiliko haya yanalenga
kuondoa kizuizi kwa baadhi ya watu ambao siyo Wabunge au Wajumbe wa Baraza la
Wawakilishi la Zanzibar au Madiwani kutoteuliwa kuwa Wajumbe wa Tume. Hata
hivyo, baada ya majadiliano, Serikali ilikubali kufanya marekebisho zaidi
kwenye kifungu hicho ili kizuizi kiwe kwa Mbunge na Mjumbe wa Baraza la
Wawakilishi la Zanzibar kama inavyoonekana kwenye jedwali la Marekebisho”.
Kinachosikitisha
ni kwamba wabunge pengine kwa kuwa na
hamu ya kutaka wawepo kwenye kamati ya
katiba , walipingana na mapendekezo ya kamati ya kutaka wabunge na wawakilishi wasiwe sehemu ya tume. Sheria
ya katiba mpya iliyofanyiwa marekekebisho bungeni ilisainiwa na Rais na kile kipengele cha kuwazuia wabunge na
wawakilishi wasiwe wajumbe wa tume kikafutwa kwa ridhaa ya wabunge katika
Mkutano wa sita tarehe 9 Februari 2012. Kwa sasa kifungu cha 6 (5) cha sheria
hiyo kinamtaka Rais Katika kufanya uteuzi wa wajumbe wa Tume kwa kutowateua watu wafuatao;
(a) mtumishi
katika vyombo vya usalama;
(b) mtu
aliyewahi kuhukumiwa kwa kutenda kosa, au ni mtuhumiwa katika shauri lililopo
mahakamani linalohusu shitaka la kukosa uaminifu au maadili; au
(c) si raia
wa Tanzania.
Ni dhahiri kuwa bunge
letu halina nguvu ya kutunga sheria wanazotaka
wanachi bali pengine sheria zingine hutungwa kwa maslahi binafsi au ya vyama. Hakukuwa na sababu ya msingi kwa
wabunge kujipigia debe kwa wao kuwa sehemu ya tume ilhali wanafahamu
wanamajukumu mengi ya kibunge.Tume ya katiba itatumia muda mwingi kukuksanya
maoni na baadaye kuandika rasimu. Sasa iweje leo wabunge msimame bungeni na
kubadilisha sheria ili Rais awateue baadhi yenu kwenye tume. Tunawashauri
wabunge wakati mwingine tuache maslahi binafsi au uchama tunapojadili mambo ya
msingi kama haya.
Hivi karibu Rais Kikwete alitangaza wajumbe 30 wa Tume hii pamoja na
Mwenyekiti wa Tume ambaye ni Jaji Sinde Warioba na Makamu Mwenyekiti Jaji Mkuu
Mstaafu Agustino Ramadhani.Wajumbe wa
tume toka Tanzania Bara wanaowawakilisha zaidi ya watu milion 40 na Mikoa si
chini ya 20 ni wajumbe15 tu.Wajumbe hawa ni Prof. Mwesiga L.
Baregu, Nd. Riziki Shahari Mngwali, Dr. Edmund Adrian Sengodo Mvungi, Nd.
Richard Shadrack Lyimo, Nd. John J. Nkolo, Alhaj Said El- Maamry, Nd. Jesca
Sydney Mkuchu, Prof. Palamagamba J. Kabudi, Nd. Humphrey Polepole, Nd. Yahya
Msulwa, Nd. Esther P. Mkwizu, Nd. Maria Malingumu Kashonda, Mhe. Al-Shaymaa J.
Kwegyir (Mb), Nd. Mwantumu Jasmine Malale Na Nd. Joseph Butiku.
Wajumbe wengine
wanaowakilisha sehemu nyingine ya nchi yenye wanachi wasiofika milion moja
(Tanzania Visiwani) nao pia ni wajumbe 15. Wajumbe hao ni Dkt. Salim Ahmed
Salim, Nd. Fatma Said Ali, Nd. Omar Sheha Mussa, Mhe. Raya Suleiman Hamad, Nd.
Awadh Ali Said, Nd. Ussi Khamis Haji, Nd. Salma Maoulidi, Nd. Nassor Khamis
Mohammed, Nd. Simai Mohamed Said, Nd. Muhammed Yussuf Mshamba, Nd. Kibibi
Mwinyi Hassan, Nd. Suleiman Omar Ali, Nd. Salama Kombo Ahmed, Nd. Abubakar
Mohammed Ali na Nd. Ally Abdullah Ally
Saleh. Kitendo cha kufanya uteuzi kwa kutokuwaangalia mtawanyiko wa wananchi kijiografia
nao umechangia kuwepo kwa watu wengi (nusu ya wajumbe) toka eneo dogo la nchi
na wanaowawakilisha wanachi wachache.
Uteuzi huu
unakinzanzana na vitu ambavyosheria ilimtaka Rais kuzingatia pale anapoteua
wajumbe wa tume. Mathalan sheria inamtaka Rais Kwa kuzingatia masharti ya
kifungu kidogo cha (3) cha sheria hii ya uundaji wa katiba mpya, muundo wa Tume
utazingatia msingi wa kuwepo kwa uwakilishi ulio sawa kwa kila upande wa
Jamhuri ya Muungano. Kosa lililofanyika ni kutafsiri neno “Uwakilishi Uliosawa”
bila kuzingatia sharti la kijiografia na mtawanyiko wa watu kama jinsi sheria
inavyosema.Hapa Uwakilishi uliosawa umechukuliwa kama vile ni lazima wajumbe
nusu watoke Tanzania Visiwani na wengine nusu Tanzania Bara.
Katika kufanya uteuzi
wa wajumbe wa Tume, Rais alipaswa kuzingatia masuala yafuatayo: uzoefu katika
kufanya mapitio ya katiba na sifa za
kitaaluma za wajumbe kwenye mambo ya katiba, sheria, utawala, uchumi, fedha na
sayansi ya jamii; pili jiografia na
mtawanyiko wa watu katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na pia umri , jinsia na uwakilishi wa makundi ya
kijamii.
Kwa muundo wa tume
suala la uwakilishi haukupewa kipaumbele
zaidi. Makundi kama ya wanawake hayana uwakilishi wa kutosha, makundi ya jamii
za pembezoni na kundi la vijana navyo pia havijapata uwakikilshi katika Tume.Vijana
ambao ndio wanamuda mrefu wa kuitumikia katiba hiyo mpya hawana uwakilishi wa
kutosha kwenye tume hii.Pamoja na kwamba kuna kigezo cha uzoefu katika suala la
sheria na katiba, bado haitoshi kuwa sababu ya kutozingatia kudi la vijana
katika tume ya katiba.
Tofauti na Mapendekezo ya Kamati ya Bunge ya Sheria
na Katiba, lakini kwa ridhaa ya wabunge
kupitia Sheria ya katiba mpya iliyofanyiwa mabadiliko Februari 2012 Rais
amewateua baadhi ya wajumbe ambao ni wabunge na wawakilishi. Wajumbe hawa ni
Mhe. Al-Shaymaa J. Kwegyir (Mb) Tanzania Bara na Raya Suleiman Hamada
mwakilishi Baraza la Wawakilishi Zanzibar. Kiuhalisia watu hawa hawakupaswa
kuwa wajumbe wa tume ya katiba kwa sababu mbalimbali zikiwemo za kuwa tayari
wanafasi kushiriki mchakato huu kwa kofia nyingine kama kushiriki Bunge la
katiba na pia wanamajukumu ya kiuwakilishi hivyo watashindwa kufanya majukumu
yao vizuri kipindi cha kukusanya maoni.
Hivyo kwa uchambuzi huu tume hii ya katiba
mpya kimsingi ina watu ambao hawakupaswa kuwa wajumbe kutokana na sababu
mbalimbali zilizoelezwa hapo juu.Wengine pia wameshatambulika na jamii kama
watu wasiopenda kuona mabadiliko ya kikatiba kwa maslahi ya umma kama
ilivyojitokeza katika kesi mbalimbali ikiwemo ya mgombea binafsi. Ni vyema
kabla ya kuanza kutenda kazi yake tume hii ikatazamwa upya.
Onesmo
Olengurumwa-Mjukuu wa Nyerere, Mjomba wa
Madiba,Mwanafunzi wa Luther King, Mfuasi wa Lenin na Mtoto wa Sokoine.
olengurumwa2@yahoo.co.uk